Kijana (18) alala mzima na kuamka kilema, Mkasa wake ni huu hapa

Huyu ndiye Bahati Charles (16) aliyezaliwa akiwa mzima wa afya njema lakini sasa ni mlemavu anayetembelea mikono na kujivuta kwa kiuno na miguu.

SIKU kadhaa zilizopita (Januari 06, 2014) tuliandika Makala iliyomhusu Mlemavu Mary Petro (51) Mkazi wa Kata ya Bupandwa wilayani Sengerema Mkoani Mwanza ambaye pamoja na ulemavu wake wa kutoweza kufanya jambo lolote katika maisha yake tangu kuzaliwa kwake,alibakwa na kupata ujauzito uliopelekea kujifungua Mtoto wa Kiume.

Hata hivyo katika hali ya kushangaza na kusikitisha mtoto huyo ambaye alizaliwa akiwa mzima huku viungo vyake vyote vikifanya kazi barabara, ghafla anajikuta naye akiwa katika hali ya ulemavu unaomfanya hivi sasa kushindwa kutimiza baadhi ya majukumu yake kwa wakati.
Ilikuwaje hadi yeye kujikuta katika hali hiyo ya Ulemavu?!.

Duniani kuna mambo, sikutegemea kwamba ipo siku ambayo ningekuja kujikuta katika hali hii niliyonayo hivi sasa, inanishangaza sana, mwanzoni sikuamini lakini imenilazimu niamini kwa sababu ndiyo yamekuwa maisha yangu kwa sasa…’.

Ndivyo anavyoanza kusimulia Mtoto Bahati Charles (18) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la Saba katika shule ya msingi Bupandwa wilayani Sengerema mkoani Mwanza ambaye ni Mlemavu anayetembea kwa mikono na kisha kujivuta kwa kutumia miguu na kiuno.

Bahati alizaliwa mwaka 1996  katika kitongoji cha Sima kijiji na Kata ya Bupandwa baada ya Mama yake Mzazi Mary kuvamiwa na kubakwa kutokana na hali yake ya ulemavu asiyeweza kufanya jambo lolote ikiwa ni pamoja na kushindwa kushika kitu chochote kwa kutumia mikono yake pamoja na miguu yake!.

Alizaliwa akiwa mzima wa viungo vyote vya mwili ingawa mama yake yeye ni Mlemavu ambapo alilelewa na Babu na Bibi yake hadi alipoanza shule, alipofika darasa la tatu aliugua Malaria kali iliyomfanya kulazwa katika hospitali ya wilaya ya Sengerema kwa wiki moja na baada ya kupona alirejeshwa nyumbani.

Nakumbuka nilikabwa sana na malaria na katika kumbukumbu zangu tangu nizaliwe sikuwahi kuugua labda wakati nikiwa mdogo lakini ninavyokumbuka tangu nilivyoanza shule sikuwahi kuugua isipokuwa wakati huo tu, nilivyoletwa nyumbani kutoka hospitali nilikaa kwa siku kama tatu hivi…’’ anasema Bahati katika mahojiano na FikraPevu.
Siku ya nne nilishindwa kuamka na kutembea kama ilivvokuwa kawaida yangu, ilipofika asubuhi nilijikuta nikiwa nimejikunja miguu kama nilivyokuwa nimelala na kila nilipojaribu kuikunjua ili kuinuka nilishindwa ikabidi nipige kelele za kuomba msaada.’’ anasema Bahati.

Anasema Babu yake alifika na kujaribu kumnyanyua na kumnyoosha miguu lakini ilishindikana, akaita ndugu na jamaa lakini pamoja na kufanya kila jitihada za kumsaidia kwa kunyoosha miguu yake ilikatalia tumboni, na tangu hapo akawa mlemavu hadi sasa ambapo anatembea kwa mikono na kujivuta kwa kutumia miguu na kiuno.

Anasema baada ya kuwa katika hali hiyo alilazimika kuacha shule na kukaa nyumbani ambapo alikuwa akibaki nyumbani na mama yake, lakini kadri siku zilizvyokuwa zikisonga mbele alikuwa akimhimiza mama yake kumpeleka shule, huku akimtaka kumuelekeza alipo Baba yake Mzazi ambaye hakuwahi kumuona tangu alipokuwa na kuelewa mema na mabaya ya ulimwengu huu,ambapo kutokana na hali hiyo ilimlazimu mama yake kumueleza ukweli.

Siku moja nikiwa nimebaki na mama yangu nyumbani Babu na Bibi wakiwa wameenda shambani mama yangu alianza kunisimulia namna ambavyo alifanyiwa na mtu asiyemfahamu hadi mimi nikapatikana…’’ anasema.

Anaongeza “Niliumia sana kwa sababu muda wote ambapo mama yangu alikuwa akinisimulia alikuwa akitokwa na machozi,lakini mimi nikajipa moyo na kumwambia mama kwamba nahitaji kusoma ili nimsaidie.’’

Anasema siku hiyo baada ya Babu yake kurejea kutoka shambani aliketi naye chini na kumweleza simulizi aliyompatia mama yake ambapo Babu yake alikiri, kisha akamuomba kuhakikisha kwamba anafanya kila jitihada za kuhakikisha kwamba anasoma, kwa sababu hakuna jambo lingine ambalo linaweza kubadilisha maisha yake yeye na mama yake tofauti na elimu.

Nilikaa kwa miaka miwili hivi nikaona Babu hataki nisome ndipo mwaka 2008 siku moja niliamua kutembea hadi katika shule ya msingi Bupandwa nikamweleza mwalimu wa ile shule kwamba nahitaji kusoma…’.
Wakati wa nyuma nilikuwa nikisoma kwenye shule hiyo nikiwa mzima wa viungo vyangu vyote hadi darasa la tatu kabla sijawa kwenye hali hii ya ulemavu,baadhi ya walimu walinikumbuka kisha wakanikubalia na kuniandikisha kuanza darasa la kwanza katika shule hiyo’’ anaeleza.

Anasema baadhi ya walimu waliokuwa wakimfundisha hapo awali katika shule hiyo akiwa mzima walishangaa kumuona kwa sababu walikuwa wakiamini kwamba alikwishafariki Dunia,na baada ya kujieleza walimu hao walimpokea na kuzungumza na mwalimu mkuu wa shule hiyo huku wakimhimiza kusoma kwa bidii.

Hata hivyo Bahati anasema amekuwa akikabiliwa na changamoto mbalimbali wakati kwenda na kutoka shuleni, ambapo wanafunzi wenzake wamekuwa wakimuona kama mtu wa ajabu na wakati mwingine hata kutompatia ushirikiano katika masuala mbalimbali ya hususani wanapokuwa darasani.

Anapokuwa njiani wakati wa kwenda ama kutoka shuleni pia amekuwa akikumbana na changamoto kadhaa ikiwemo na kutokusaidiwa na jamii hata kwa kubebwa tu na baiskeli, wengi wamekuwa wakimpita njiani na kumuona kama mtu fulani wa ajabu katika eneo hilo.

Kuna baadhi ya watu ni kama vile wananiogopa, nadhani ni kwa sababu siku na hali hii ya ulemavu huko nyuma, ni jambo ambalo limenitokea ghafla, kwa hiyo limewastua na linaendelea kuwastua watu wa hapa kijijini…’’ anasema Bahati.

Kifungu cha 8.(1) cha sheria ya Mtoto iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2009 kipengele cha wajibu wa Kumtunza mtoto(Duty to maintain a Child) kinasema Itakuwa ni wajibu wa mzazi au mlezi kumtunza mtoto na huo wajibu wa mzazi au mlezi unampa mtoto haki ya:

  • Chakula
  • Malazi
  • Mavazi
  • Huduma za afya pamoja na chanjo
  • Elimu na malezi
  • Uhuru
  • Haki ya kucheza na kuburudika.

Aidha kifungu hicho cha 8 (2). Kinasema mtu yeyote hatamnyima mtoto kupata elimu, chanjo, chakula, mavazi, malazi, huduma ya afya na matibabu au chochote kinachohitajika kwa maendeleo ya mtoto.

Kwa Mtoto Bahati pamoja na maelekezo haya ya vifungu vya sheria hiyo ya mwaka 2009 anasema hakuna anachokipata kutoka kwa wazazi ama walezi ama mtu yeyote ambaye amekuwa akikutana naye katika maeneo mbalimbali kijijini hapo.

Namjua mzazi wangu mmoja tu ambaye ni mama, Baba yangu simjui kwa sababu mama aliniambia hata yeye hamjui kutokana na namna alivyotendewa,kuna majirani, watu mbalimbali katika eneo tunaloishi, lakini inavyoonekana hapa kwetu wanapaogopa kwamba ni kwa wachawi ndio maana tunakumbana na matatizo kama haya……’’ anaeleza. 

 Hii ndiyo hali halisi ya mama yake mzazi na Bahati aliyebakwa na kisha Kumzaa Bahati.

UWEZO WAKE DARASANI

Waswahili wanasema Mwenyezi Mungu hawezi kukunyima vyote: Bahati ni Mlemavu anayetembea kwa kutumia mikono huku akijivuta kwa miguu na kiuno ambapo analazimika kutumia muda wa masaa 3 kutoka nyumbani hadi kufika shuleni, lakini anawashangaza walimu wake pamoja na wanafunzi wenzake kutokana na uwezo wake darasani.

Katika Darasa lao la saba walikuwa jumla ya wanafunzi 136 lakini yeye akiwa anashika nafasi ya sita katika matokeo ya mtihani na hasa ikizingatiwa kwamba katika darasa lao yeye pekee ndiye Mlemavu, huku wanafunzi wenzake wote wakiwa ni wenye viungo kamili, hali ambayo anasema kuna wakati imekuwa ikimtia simanzi ingawa anaamini kwamba hali aliyo nayo ni Changamoto tu katika maisha ya kila siku.

Kuna wakati nawaona wenzangu wakinishangaa sana lakini kibaya zaidi kuna wengine wanafikia hatua ya kunicheka na kunisimanga na kunitania kutokana na ulemavu wangu, lakini huwa nawapa msemo mmoja unaosema ‘Hujafa Hujaumbika’.
Binafsi sijapenda kuwa katika hali kama hii lakini ni changamoto tu za kibindamu ndizo zimenifikisha hapa nilipo, ipo siku hata wao wanaweza kujikuta katika hali kama hii pengine zaidi ya hii niliyonayo” anasema Bahati.
Nasema hivyo kwa sababu mimi binafsi sikuwa  na ulemavu kama huu nilikuwa mzima kabisaa,lakini cha ajabu leo hii mimi ni mleamvu tena sio ulemavu wa ajali ya gari, baiskeli au Pikipiki, lakini ni ulemavu uliokuja kutoka sehemu ambayo hakuna mtu yeyote ambaye anajua hadi leo hii,ni miujiza tu na mimi nimelazimika kukubaliana na hali hii kutokana na uhalisia wake.” anaongeza.

Bahati anasema pamoja na kuwa katika hali hiyo kwa miaka mingi lakini hakuna mtu yeyote ambaye amekwishajitokeza kwa ajili ya kumsaidia, ikiwa ni pamoja na kumpatia nguo za shule,madaftari pamoja na mahitaji mengine, ambapo amekuwa akijihusisha na biashara ya kutengeneza Nyavu za kuvulia samaki ambayo ndio imekuwa ikimuwezesha kupata mahitaji yake madogo madogo.

Kila ninapozungumza na mama anaonekana kabisa ni mtu ambaye amekata tamaa ya maisha na anachosubiri hivi sasa ni kifo tu,maneno yake haya yamekuwa yakinitia huzuni na maumivu makali sana moyoni…’’ anasema na kuongea.
Ndiyo maana nataka nisome sana na kubwa kama mungu akinisaidia nitasomea sheria ili niweze kupambana na wabakaji, hawa ni wauaji, wamembaka mama yangu asiyejiweza, wamempa mimba, nimezaliwa, nimekuwa mlemavu na sasa nahangaika na mama yangu wao wapo wamekaa kimya, inaumiza sana…” anasema Bahati huku akifuta machozi machoni.
Babu na Bibi ambao ndio walikuwa walezi wakuu wa mama yangu na mimi wamefariki Dunia, Mama yangu Mkubwa aliyemchukua mama na mimi kwa ajili ya kutulea naye amefariki Dunia mwaka jana…’’anafafanua.

Anaongeza “Hapa mimi na mama tumebaki peupee wanaomlea mama sasa ni watoto wadogo wa mama mkubwa ndio wanamsaidia, lakini nao ni wanafunzi, ni wazi kwamba picha iliyoko mbele ya mama yangu na hata mimi ni hatari tupu……ila naamini Mungu yupo atafanya kazi yake…..’’. 

 Anasema hitaji kubwa kwake kwa sasa ni kupata Baiskeli maalum wanayotumia walemavu ambayo anaamini akiipata itamsaidia sana katika kuendesha shughuli zake na hasa katika masomo yake,kwa sababu kilicholemaa ni miguu yake lakini mikono yake inafanya kazi hivyo anao uwezo wa kutumia mikono yake katika kuendesha baiskeli hiyo maalum ya walemaavu.

Mwalimu Mkuu wa shule anakosoma Bahati Simon Masami anakiri kuwepo kwa mwanafunzi huyo katika shule yake pamoja na mateso mbalimbali anayoyapata ikiwa ni pamoja na umbali anakotoka hali ambayo imekuwa ikimsababisha kila siku kuchelewa shuleni na hivyo kukuta wenzake wamemaliza vipindi viwili ama vitatu.

Anasema pamoja na kwamba mwanafunzi huyo anaonekana kuwa katika mazingira magumu, lakini amekuwa mfano kwa wananfunzi wengine kutokana na kujituma kwake katika masomo.

Kuna matatizo tu madogo madogo kutoka kwa badhi ya wanafunzi wenake ambao wamekuwa wakimuona tofauti, kwa sababu wengine wanamfahamu tangu zamani akiwa mwenye viungo vyote, sasa hali iliyomkuta inawastua na kuwagopesha wengine,na kibaya sana watu wengi wa huku wanamini zaidi masuala ya kishirikina….’’ anasema Mwalimu katika mahojiano na FikraPevu.
Lakini ni kijana mwenye akili sana darasani,mara nyingi nimekuwa nikimshauri kujitahidi sana katika masomo yake na nimefikia hatua hadi wakati mwingine kumruhusu kusoma na nguo za nyumbani pale ambapo anakuwa bado hajapata wasamaria wema wa kumsaidia,lakini ukweli ni kwamba ni mtu ambaye anahitaji kusaidiwa kwa kila hali na hasa ikizingatiwa kwamba mazingira yetu tunayoishi ni ya kijijini sana….’’ anasema Mwalimu Mkuu wa shule hiyo.

Diwani wa Kata ya Bupandwa anakoishi Mlemavu huyo anasema amekuwa akijitahidi kumsiaida badhi ya vifaa vya shule, lakini bado hali ni ngumu kwake na hasa katika suala zima la mavazi, pamoja na baikeli.

Kuna vifaa ambavyo gaharama yake ni kubwa kama vile Baiskeli zile wanazotumia walemavu, nasikia gharama yake ni pesa zisizopungua 120,000/=, sasa kwa maisha ya kijijini ni ngumu sana, kama kuna watu wanaoweza kujitokeza kumsaidia kupata vitu kama hivyo ajitokeze….’’ anasema Diwani Masumbuko.

Mama Mzazi wa mwanafunzi Bahati ambaye pia ni Mlemavu asiyejiweza katika kufanya jambo lolote kwa kutumia viungo vya mwilini mwake, anasema mwanaye amekuwa akiteseka na hakuna mtu ambaye amekwishajitokeza kumsaidia.

Unavyoniona mimi ni mlemavu, tena bora hata ya huo wa mwanangu Bahati, bora yeye ana uwezo wa kutembea kwa kujivuta, mimi hata kujigeuza siwezi, nateseka, naye anateseka, ndiyo maisha ya Duniani…..’’ anasema na kuongeza.
Nilimzaa akiwa mzima kabisa bada ya kupata yale matatizo ya kubakwa na mtu ambaye sijamfahamu hadi sasa, akakua vizuri mpaka akaanza shule, alipofika darasa la tatu akaugua malaria, akapona alipoletwa nyumbani siku moja tukaamka na kumkuta akiwa kwenye hali hiyo….’’.

Anasema yeye amekwishakata tamaa na maisha na anachosubiri ni kifo, na kwamba amekuwa akimsihi mwanaye kukazania masomo yake, akiamini kwamba elimu pekee ndiyo ambayo huenda siku moja ikaja kumsaidia katika maisha yake.

Mama mzazi wa Bahati ni mlemavu wa viungo vya mwili ambapo mikono yake imekunjamana kifuani,huku miguu yake ikiwa imepinda kwa kutoka nje, ambapo tangu kuzaliwa kwake akiwa na miaka 51 hivi sasa hajawahi kushika kitu chochote,hajawahi kulala kifudifudi, na wala hajawahi kulala ubavu, bali analala chali kwa muda wote.

Baadhi ya wanafunzi waliozungumza na FikraPevu wanasema wameshangazwa na hali iliyomkuta mwenzao ambaye awali alikuwa mwenye afya nzuri na mzima wa viungo vyote lakini kwa sasa amebadilika, hali ambayo wakati mwingine imekuwa ikiwaogopesha.

Kifungu cha 5(1) Cha sheria ya mtoto ya mwaka 2009 kinachozungumzia Haki ya kutobaguliwa (Non-discrimination),kinasema Mtoto ana haki ya kuishi huru bila kubaguliwa,ambapo katika kifungu cha (2),kinafafanua kuwa Mtoto ana haki ya kutobaguliwa kwa misingi ya rangi, kabila, dini, maoni ya kisiasa, ulemavu, hali ya kiafya, desturi, wa mjini au kijijini, kuzaliwa, hali ya kijamii na kiuchumi, mkimbizi au hali yeyote ile.

Kuna haja ya Watanzania kuacha unyanyapaa ambao unawatenga walemavu na kuwakosesha wengi wao furaha za maisha, haki zao, elimu, ajira, umiliki wa mali, nguvu za kiuchumi na uongozi katika umma. Maumbile yao yasiwe kikwazo cha kuiona dunia chungu. Kujiona viumbe waliokosa upendo. Katika nchi nyingine tayari wamekwisha kuliona hili, vyoo vya umma vimejengwa vikitenga sehemu za walemavu, sheria za vyombo vya usafiri nazo zimelenga kuwasaidia. Ipo haja kwa Tanzania kulitilia shime hili na kuona linafanyika. Tatizo kwa walemavu halipo katika vyombo vya usafiri pekee, bali hata katika sekta ya ajira na mahusiano, na msomi, kwa sababu ya ulemavu wake inakuwa tabu kupata kazi na wasichana walemavu wanaambulia kupewa mimba na kutelekezwa, watoto wananyimwa fursa ya kujiunga katika baadhi ya shule kutokana na ulemavu wao.

Kwa mujibu wa sera ya Taifa ya Maendeleo na huduma kwa watu wenye ulemavu, Ulemavu ni hali inayotokana na dosari ya kimwili au ya kiakili ya muda mfupi au ya kudumu ambayo inampunguzia mtu uwezo na fursa sawa katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali katika jamii.Upungufu huo unaweza kuchochewa na mazingira na mtizamo wa jamii kuhusu ulemavu.

Credit Fikra Pevu.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s