Tunajifunza nini kutokana na mfanyakazi wa ndani aliyeonyesha ukatili kwa mtoto kule Uganda?

Tumekuwa na hisia tofauti na maneno tofauti tofauti kuhusu kitendo cha mfanyakazi wa ndani Jolly Tumuhirwe wa nchini Uganda aliyemfanyia ukatili mtoto mdogo, Arnella Kamanzi. Mara nyingi jamii zetu huwa tunaangalia kwa juu juu tu mambo yanapotokea bila kuangalia chanzo cha tukio hilo ni nini? Mwanasaikolojia mmoja aliyetoa maelezo yake kwa kusema inawezekana kabisa ni mazingira ya makuzi aliyokulia huyo binti, kuhusiana na chuki, manyanyaso aliyopitia na hata yakasababbisha kufanya kazi aliyonayo sasa.

Kitu cha Msingi ni kwamba tunajifunza nini? Mambo ya kuangalia ni kwamba thamani ya maisha yetu walio wengi tunathamini kazi na biashara zetu kuliko familia tulizonazo. Kutokana na hayo tumekuwa tukiishi na wafanyakazi wa ndani kwa kutokuwatilia umuhimu mkubwa na kutojua thamani yao katika familia zetu. Mimi sio mwanasheria hivyo sitoweza kugusia kisheria na mambo yanayoambatana na hayo, bali wazazi kuna nafasi kubwa ya kulaumiwa kutokana na mambo yanayoendelea majumbani mwetu.

Je unaishi vipi na Mfanyakazi huyo?  Ukienda kwenye nyumba nyingi zenye wafanyakazi wa ndani utagundua kuwa huwa wanaishi maisha magumu kuliko hata unavyofikiri. Kitu cha kwanza wao ndio wa kwanza kuamuka  na wa mwisho kulala. Kazi wanayofanya mara nyingi haiendani na kipato wanacholipwa. Vile vile namna ambavyo wanachukuliwa ni bila heshima kabisa. Unaweza kujiuliza kama una house girl au mfanyakazi wa ndani ni mara ngapi umekula chakula pamoja naye mezani unapokula na familia yako?

Mara zote tunafikiri wao wanastahili mshahara mdogo, haawatakiwi kula vizuri au kukaa mahali pazuri na kuwatumia kama mashine fulani hizi ambayo haina hisia hata kidogo. Mambo mengi kama hayo yanasababisha wao kuanza kufanya vitu vya ajabu kuona kwamba hawana thamani bali ni kutumiwa tu kama mashine.

Familia hiyo ina majibu ya kutosha kuhusiana na tukio hilo, kwa hali ya kawaida haiwezekani mtu akafanya ukatili wa namna fulani bila sababu. Ingawa wengine wana hulka tofauti sana za utu, nina marafiki zangu huwa tuna utani huu ukiona mtu anakuadhibu kuliko kosa ulilofanya kwa wakati huo inamaanisha kuna kitu zaidi ya kosa hilo.

Najua kuna wengine huwa wanafikiri wanawatendea vizuri mabinti hao, bali matokeo tunayokutana nayo hutupa majibu ya kuwa kama tunawatendea vyema au la! Kuna wale ambao wanawatendea vizuri na kupata matokeo mazuri kwenye familia, hao wapo kabisa na ushahidi wengine tunao. Unachotakiwa kujua ni kwamba unachopanda ndicho unachovuna, hivyo kisasi wakati mwingine wanashindwa kurudisha kwako wewe  kwakuwa una nguvu hivyo wanatafuta wapi kwa kumalizia hasira zao. Watoto wako wako hatarini kutokana na matendo yako ya kinyanyasaji juu ya wadada wa kazi.

Hebu fikiri kwamba, humwamini mfanyakazi wako na funguo ya gari ila una mwachia nyumba pamoja na watoto wakati huo huo ndiye atakayekupikia chakula. Hii inamaanisha maisha na uhai wako uko mikononi mwa mfanyakazi wa ndani ambaye inawezekana ameishia darasa la saba tu. Akili ni nywele kila mtu ana zake, simaanishi kwamba napuuzia kile kilichotokea la hasha bali kila jambo hutokea ili tujifunze kwa undani. Inawezekana huyo binti akaadhibiwa na kupoteza kazi yake, kama kuna kitu ambacho ameendelea kutendewa na hakikurekebishwa kwenye familia hiyo inamaanisha kwamba mfanyakazi wa ndani mwingine kama akiletwa anaweza kutendewa hivyo hivyo. Mara hizi zote hatuonyeshwi upande wa pili wa shilingi, tunachoona ni makosa ya huyo binti kwangu mimi nitajiuliza kwanini aliamua kufanya hivi? Hapo ndipo tunaweza kugundua chanzo na kurekebisha makosa hayo.

Kama kuna kitu umejifunza, je thamani ya watoto wako ikoje kulinganisha na kazi yako? Kitu gani kinakufanya au kutufanya tuajili mtu mwenye elimu ya chini zaidi ndiye atunze familia zetu? Maisha ya watoto wetu yanategemea malezi ya nani? Kazi kwako, fanya maamuzi magumu kuokoa kizazi chako la sivyo unahitaji kufikiri kwa mapana na malefu zaidi kabla ya kuhukumu na kumlaani binti huyo. Mimi najaribu kufikiri zaidi ya tukio hilo bila kupunguza ukubwa na kitu kilichotokea kwa mtoto. Ninawapa pole familia na mtoto aliyekumbwa na unyama huo, Mungu aendelee kumpa ahueni na kuyanusuru maisha yake.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s