Saratani ya tezi dume ni hatari

Pamoja na maelezo ya Rais Jakaya Kikwete aliyotoa juzi juu ya ugonjwa wa saratani ya tezi dume mara baada ya kurejea nchini kutoka Marekani alikotibiwa, maswali kuhusu ugonjwa huo bado ni mengi na hivyo kuhitaji ufafanuzi.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere mara baada ya kuwasili nchini, Rais Kikwete alielezea hali yake, jinsi alivyogundulika kuwa na saratani ya tezi dume na matibabu aliyoyapata.

Rais Kikwete anastahili pongezi kwa namna alivyovunja ukimya na amesaidia kujua umuhimu wa kujali afya zetu na kuweka wazi hali zetu za kiafya, si kwa tezi dume pekee, bali pia maradhi mengine.

Maana ya saratani

Saratani maana yake ni ukuaji holela bila mpangilio wa seli baada ya kuparanganyika kwa mfumo wa seli unaodhibiti ukuaji na uhai wake. Na uvimbe wa kawaida wa tezi maana yake ni kuwa seli zimetutumka tu lakini hakuna mparanganyiko wa seli wala kukua kwa kusambaa kiholela kama ilivyo kwa saratani.

Hivyo, ndio maana kuna tatizo la kuvimba tezi dume na wengine kupata saratani ya tezi dume kwa wanaume wenye umri mkubwa.

Tezi dume ni sehemu mojawapo ya mfumo wa uzazi wa kiume. Inaundwa na sehemu mbili ambazo zimeunganishwa na kufunikwa kwa nje kwa utando wa tishu.

Tezi hii ipo mbele kidogo ya puru (rectum) na chini kidogo ya kibofu cha mkojo. Tezi dume inauzunguka mrija unaounganisha kibofu cha mkojo na uume (urethra).

Kazi ya tezi dume

Mojawapo ya kazi za tezi dume ni kutoa majimaji yanayochanganyika na mbegu za kiume (sperms) wakati wa kilele cha tendo la kujamiana. Mchanganyiko huu wa mbegu pamoja na majimaji hayo hutengeneza shahawa (semen).

Majimaji hayo husaidia kuzipa mbegu za kiume nguvu ya kusafiri kwenye uke mpaka kufikia kwenye mirija ya uzazi, tayari kwa utungisho na yai la kike. Vilevile husaidia kupunguza hali ya kitindikali iliyopo katika uke, ambayo isiporekebishwa, huua mbegu nyingi za kiume na kufanya utungisho kuwa wa tabu.

Saratani ya tezi dume inashika nafasi ya tatu kwa kusababisha vifo vinavyotokana na saratani kwa wanaume wa umri mbalimbali duniani.

Saratani ya aina hii kwa wanaume inashika nafasi ya kwanza Tanzania kwa kusababisha vifo. Pia ni chanzo kikuu cha vifo vinavyosababishwa na saratani kwa wanaume wenye umri wa kuanzia miaka 70 na kuendelea. Hata hivyo, ni nadra sana kwa saratani hii kuwapata wanaume chini ya miaka 40.

Nani yupo hatarini?

Watu walio katika hatari kubwa ya kupata saratani ya tezi dume ni pamoja na wanaume wenye asili ya Afrika (weusi) ikilinganishwa na Wazungu, wanaume kuanzia miaka 60 na kuendelea, wanaume wenye historia ya tatizo hili kwenye familia zao, yaani wale ambao mmoja wa ndugu zake (kaka au mdogo wa kiume) au baba amewahi kuugua ugonjwa huu.

Wanaume wanaokunywa pombe na utumiaji tumbaku kupindukia, wanaofanya kazi kwenye viwanda vya kutengeneza rangi au wanaofanya kazi ya kupaka rangi, waliowahi kupata maambukizi ya tezi dume na wakulima wanaotumia aina fulani ya mbolea za kemikali.

Pia wanaofanya kazi kwenye viwanda vya utengenezaji matairi, wachimbaji wa madini, hususan aina ya cadmium, walaji wa chakula chenye kiasi kikubwa cha mafuta, hasa ya wanyama.

Pamoja na kwamba, tatizo la kukua na kuongezeka kwa tezi dume yaani BPH hutokea kwa wanaume wengi, hali hiyo haiongezi hatari ya kupata saratani ya tezi dume.

Dalili za saratani ya tezi dume

Katika hatua zake za awali, dalili za saratani ya tezi dume hazitofautiani sana na zile za kuvimba kwa tezi dume (BPH). Dalili hizo ni pamoja na kupata shida unapoanza kukojoa, kutiririka mkojo baada ya kumaliza kukojoa, kutoa mkojo wenye mtiririko dhaifu, kukojoa mara kwa mara hasa nyakati za usiku, kujikakamua wakati wa kukojoa na kushindwa kumaliza mkojo wote, kutoa mkojo uliochanganyika na damu na kutoa shahawa zilizochanganyika na damu.

Iwapo saratani imesambaa mwilini kiasi cha kuhusisha sehemu za jirani ya mwili, mgonjwa anaweza kuwa na maumivu makali ya mifupa katika maeneo ya nyonga, mapajani na kiunoni, uume kushindwa kusimama na mgonjwa huwa na dalili nyingine zinazoweza kumpata mgonjwa mwingine yeyote wa saratani kama vile kupungua uzito, kuhisi kichefuchefu, uchovu na kizunguzungu.

Vipimo saratani ya tezi dume

Utambuzi wa saratani ya tezi dume hujumuisha kufahamu historia ya mgonjwa pamoja na familia yake, kufahamu dalili alizonazo mgonjwa pamoja na kufanya vipimo kadhaa. Vipimo vinavyoweza kufanywa ni pamoja na:

Kidole

Uchunguzi kwa kutumia kidole cha shahada iitwayo digital rectal examination (DRE): Daktari ataingiza kidole cha shahada katika puru (rectum) ili kuhisi tezi dume kupitia ukuta wa puru. Aidha atahisi pia sehemu zote zinazozunguka tezi dume kutambua iwapo tezi ni ngumu au kama ina uvimbe wowote.

Kipimo hiki ndicho rahisi kinachokubalika duniani kote na kisicho na gharama cha kugundua tatizo mapema, lakini kimekuwa kikipata upinzani mkubwa kutoka kwa wagonjwa kutokana na imani potofu na kutokuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu kipimo hiki wakidhani ni cha udhalilishaji wa uanaume wao.

Daktari hukupa taarifa kuhusu kipimo na hufuata maadili wakati wa upimaji.

Damu

Kipimo cha damu kuchunguza aina ya protein inayozalishwa na seli za tezi dume kiitwacho Prostate Specific Antigen (PSA): PSA ni uzalishaji wake huongezeka wakati wa BPH, tezi dume inapopata uambukizi (prostitis) na saratani ya tezi dume.

DRE na PSA huonyesha kuwapo kwa tatizo kwenye tezi dume, lakini vipimo hivi havina uwezo wa kutofautisha iwapo tatizo hilo linamaanisha saratani au BPH.

Prostate Biopsy

Ili kutofautisha kati ya magonjwa hayo, kipimo kiitwacho Prostate Biopsy hufanywa. Kipimo hiki hufanywa kwa kuchukua kipande cha nyama (tishu) kutoka tezi dume kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara.

Transrectal ultrasound

Kipimo kingine huitwa transrectal ultrasound ambacho husaidia kuonyesha ukubwa na sura ya tezi dume lilivyo. Ili kutambua kama saratani imesambaa sehemu nyingine za mwili vipimo vya CT scan, MRI pamoja na PET navyo vyaweza kufanyika pia.

Tiba

Kuna njia kadhaa za matibabu ya saratani ya tezi dume. Hata hivyo, uamuzi wa njia gani itumike unategemea ushauri na maoni ya daktari kulingana na hatua ya ugonjwa ulipofikia na umri wa mgonjwa.

Kwa ujumla, saratani ina hatua ya kwanza, ya pili, ya tatu na ya nne. Katika hatua za awali za ugonjwa, daktari anaweza kushauri mgonjwa atibiwe kwa kufanyiwa upasuaji na tiba ya mionzi, wakati kwa wagonjwa wazee, daktari anaweza kushauri kumfuatilia mgonjwa kwa ukaribu bila kumfanyia upasuaji au bila kumpatia tiba ya mionzi.

Iwapo saratani imesambaa na kuathiri sehemu nyingine za mwili, matibabu yake yanaweza kujumuisha upasuaji wa kuondoa korodani, matumizi ya dawa za kupunguza kiwango cha homoni ya testosterone katika damu (hormonal therapy) au matumizi ya kemikali za kuua seli za saratani (chemotherapy).

Upasuaji

Upasuaji hufanyika kwa wagonjwa walio katika hatua za awali za ugonjwa (hatua ya kwanza na pili) ingawa pia hufanywa kwa baadhi ya wagonjwa walio katika hatua za mwisho za ugonjwa huu, yaani hatua ya tatu na nne. Upasuaji unaofanywa ni ule wa kuondoa tezi dume pamoja na baadhi ya tishu zinazozunguka tezi hiyo.

Upasuaji unaweza kuwa wa njia ya zamani kwa kupitia sehemu ya chini ya kitovu, upasuaji wa kutumia kifaa maalumu kinachoingizwa katika njia ya mrija wa mkojo na upasuaji wa njia ya kisasa yaani upasuaji matundu madogo na kuingiza kifaa chenye kamera, kisu chenye uwezo wa kukata na kuchomelea mishipa ya damu ili isivuje na kikapu cha kupakulia tishu zilizokatwa.

Madhara yanayoweza kujitokeza ni pamoja na uvujaji damu kupita kiasi, maambukizi, maumivu, kupungua au kupotea kwa nguvu za kiume, ugumba kama ikitokea vijeraha wakati wa upasuaji na mbegu za kiume kumwagikia katika kibofu cha mkojo.

Lakini upasuaji wa kisasa umefanikiwa kupunguza madhara haya kwa kiasi kikubwa.

Tiba ya mionzi

Hii ni aina ya tiba inayotumia mionzi kuua seli zenye saratani. Tiba ya mionzi hutumika kutibu saratani ya tezi dume ambayo haijasambaa kwenye sehemu nyingine za mwili. Aidha inaweza pia kutumika kuua masalia ya tishu zenye saratani mara baada ya kufanyika kwa upasuaji.

Kwa wagonjwa walio katika hatua ya mwisho ya saratani, yaani wale ambao saratani tayari imeshasambaa mwilini, mionzi hutumika kupunguza maumivu makali ya mifupa.

Madhara anayoweza kupata mgonjwa kutokana na aina hii ya tiba ni pamoja na kushindwa kusimamisha uume au uhanithi, kukosa hamu ya kula, uchovu, ngozi kubabuka, kuharisha na kutoa mkojo uliochanganyika na damu.

Tiba ya vichochezi (Homon)

Hii ni aina ya tiba inayotumia dawa zinazopunguza kiwango au ufanyakazi wa homoni ya testosterone mwilini. Testosterone ni homoni ya kiume inayochochea ukuaji wa tezi dume, hivyo basi matumizi ya dawa hizi husaidia kupunguza ukuaji huu na kusambaa kwa seli za saratani.

Tiba ya homoni hutolewa kwa wanaume walio katika hatua za mwisho za ugonjwa huu kwa nia ya kupunguza maumivu na kutibu dalili za ugonjwa. Dawa zinazotumika kwa tiba ya aina hii zimegawanyika katika makundi mawili, zile zinazochagiza uzalishaji wa homoni ya luteinizing na zile zinazozuia ufanyaji kazi wa homoni ya androgen.

Madhara yanayoweza kusababishwa na utumiaji wa dawa hizi ni pamoja na kichefuchefu na kutapika, upungufu wa damu, kuongezeka uzito, uhanithi na kukosa hamu ya tendo la ngono, matatizo katika ini na matiti kuwa makubwa.

Baadhi ya madaktari hutumia upasuaji wa kuondoa korodani kama njia ya kupunguza kiwango cha homoni za kiume mwilini kwa kigezo kwamba kiwango kikubwa cha homoni hizi huzalishwa kwenye korodani. Hata hivyo tiba hii haifanyiki mara kwa mara.

Credit Mwanachi

Follow us on
Facebook: http://facebook.com/tubongetz
 Twitter: http://twitter.com/tubongetz
  Instagram: http://instagram.com/tubongetz

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s