Fahamu hapa kuhusiana na Ugonjwa wa zinaa wa Chlamydia

CHLAMYDIA NI NINI?

Chlamydia ni aina ya ugonjwa wa zinaa unaosababishwa na bakteria aina ya chlamydia Trachomatis, ambao wanaweza kuathiri viungo vya uzazi na pia kusababisha ugonjwa wa homa ya mapafu unaojulikana kama typical pneumonia.

Kati ya magonjwa ya zinaa yanayosababishwa na bakteria, chlamydia ndio ugonjwa unaoongoza kwa maambukizi duniani ambapo nchini Marekani pekee inakisiwa watu milioni 4 huambukizwa ugonjwa huo kila mwaka.

Inawezekana jina la ugonjwa huo halijazoeleka katika masikio ya wengi na hii huenda ni kutokana na kutokuwepo kwa takwimu za kutosha kuhusiana na suala hilo katika nchi nyingi barani Afrika na hasa katika nchi zetu za Afrika Mashariki, hivyo ni vigumu kujua idadi kamili ya maambukizi. Lakini bila shaka chlamydia ndio ugonjwa wa zinaa unaotokana na bakteria unaoongoza kwa maambukizi mengi zaidi duniani ukifuatiwa na ugonjwa wa gono.

Gonjwa hili ambalo huwaathiri wanawake na wanaume pia linaweza kuleta madhara makubwa ikiwa ni pamoja na kuharibu mfumo wa uzazi wa mwanamke. Nchini Marekani pekee mwaka 2011, kesi milioni 1 na nusu ziliripotiwa katika hospitali katika majimbo 50 ya nchi hiyo, katika hali ambayo kesi nyingi hazikuripotiwa kwa kuwa watu wengi wenye kuambukiza ugonjwa huo huwa hawaonyeshi dalili na hivyo huwakwenda hospitali.

Kama yalivyo magonjwa mengi ya zinaa, chlamydia pia huwapata zaidi vijana na takwimu zinaonyesha kuwa kati ya wasichana walio na umri wa miaka 14 hadi 15 wenye kufanya ngono zembe mara kwa mara, mmoja wao huambukizwa chlamydia.

Ugonjwa wa chlamydia huweza kuambukizwa kupitia njia za kujamiana. Mtu yoyote mwenye kufanya ngono zembe na mtu aliye na ugonjwa huo anaweza kuambukizwa.

Pia mama mjamzito huweza kumuambukiza mtoto wake wakati wa ujauzito. Vile vile ugonjwa huo wa zinaa unaweza kuambukizwa kupitia  mbwa, vinyesi vya wanyama kama vile ndege walioambukizwa aina ya Chlamydia inayopatikana kwa wanyama  kwa mfano kuku, bata, kasuku na kadhalika na kusababisha aina ya homa ya mapafu inayojulikana kama psittacosis ambayo huambatana na homa kali yenye nyuzi joto kati ya celsius 39.4  hadi 41.1.

Chlamydia huathiri sehemu tofauti za mwili wa binadamu kama macho, mfumo mzima wa kupumua, sehemu za siri, viungo vya uzazi na tezi (lymph nodes).

JE, DALILI NA VIASHIRIA VYA UGONJWA WA CHLAMYDIA NI ZIPI?

Asilimia 75 ya wanawake na asilimia 50 ya wanaume wanaopata maambukizi ya ugonjwa huu huwa hawaonyeshi dalili zozote za ugonjwa huo.
Dalili hutokea wiki 1 hadi 3 baada ya mtu kupata maambukizi.

WANAWAKE WANAWEZA KUONYESHA DALILI ZIFUATANO:

 1. Kutokwa na majimaji ya rangi ya njano yanayotoka kwenye utupu, ambayo huwa na harufu kali.
 2. Kuhisi maumivu wakati wa haja ndogo.
 3. Kuhisi kama kuwaka moto wakati wa kukojoa.
 4. Kutokwa na damu katikati ya kipindi cha hedhi yaani baada ya kumaliza mzunguko wa hedhi na kabla ya kuanza mzunguko mwengine.
 5. Kuhisi maumivu sehemu ya chini ya tumbo.
 6. Kuhisi maumivu wakati wa kujamiana.
 7. Kutokwa na damu wakati wa kujamiana na pia kuvimba na kuhisi maumivu kwenye tezi zilizopo sehemu za siri.

DALILI KWA WANAUME ZINAWEZA KUWA NI:

 1. Kuhisi maumivu wakati wa kukojoa.
 2. Kuhisi kama kuwaka moto wakati wa kukojoa.
 3. Kutokwa na majimaji kwenye uume ambayo yanaweza kuwa ya rangi nyeupe kama maziwa, kijivu au rangi ya njano.
 4. Sehemu ya tundu kwenye uume kuwa nyekundu, kuvimba na kuwasha.
 5. Kuhisi maumivu kwenye korodani na tezi zilizopo sehemu za siri ambazo huvimba na kuambatana na maumivu. Mara nyingi dalili hizi kwa wanaume hukuja na kupotea au zinaweza kuonekana tu wakati anapoenda kukojoa asubuhi baada ya kuamka kutoka usingizini.
Dalili za ugonjwa huu kama umeathiri puru/mkundu (rectum) kwa wanawake na wanaume ni kama ifuatavyo:
Kuwashwa na kutokwa na damu kwenye puru/mkundu,
maumivu wakati wa kujisaidia haja kubwa na kutokwa na uchafu kama kamasi kutoka kwenye puru/mkundu.
Iwapo vimelea vya chlamydia vitaathiri macho,
wanawake na wanaume huwa na dalili zifuatazo:
Uvimbe kwenye macho, macho kuwa mekundu,
kuwasha na hata kutokwa na majimaji machoni.
Chlamydia inayoambukiza kwenye macho (Chlamydia conjunctivitis or trachoma) ndiyo inayoongoza kwa kusababisha upofu duniani.
Baada ya mtu kuhisi dalili hizo tulizozitaja, hupaswa kwenda hospitalini au katika kituo cha afya ili kupimwa na kuthinitishwa kwamba ana ugonjwa huo ili apatiwe matibabu.
Vipimo vya uchunguzi vya ugonjwa wa Chamydia ni Urethral swab for culture.
Katika kipimo hiki maji maji kutoka kwenye uume au uke huchukuliwa kwa kutumia kijiti chenye pamba au swab maalum ambayo hupelekwa maabara ili kuoteshwa na kuangalia aina ya uoto wa bakteria.
Pia huchukuliwa vipimo vya mkojo na pia kipimo cha PCR au Polymerase Chain Reaction, ambacho ni cha kuangalia vinasaba vya bakteria au DNA na hufanywa katika maabara.
Baada ya majibu kuonyesha kuwa mgonjwa ameambukizwa vimelea vya ugonjwa huo matibabu hufuata. Chlamydia ni kati ya magonjwa ya zinaa yanayotibika na ugonjwa huu hutibiwa kwa dawa aina ya antibiotiki zilizopo kwenye makundi ya macrolides, Quinolones na Polyketides ambazo hutolewa chini ya maelekezo ya daktari.

MADHARA YA UGONJWA HUU NI YAPI?

Mpenzi msomaji madhara ya ugonjwa huu kwa wanaume,
ni kuwa huathiri korodani na kusababisha mwanamume kukosa uwezo wa kuwa na watoto au kuwa tasa na pia husababisha maambukizi kwenye tezi dume (prostatitis).

Kwa wanawake.

husababisha maambukizi kwenye mirija ya uzazi, mfuko wa uzazi, na mayai ya uzazi, kwa hivyo kusababisha ugonjwa wa uvimbe katika fupanyonga au Pelvic inflammatory disease (PID).
Pia huongeza uwezekano wa wanawake kupata mimba zinazotunga nje ya mfuko wa uzazi ambazo kitaalamu hiutwa Ectopic pregnancy. Mbali na hilo, mwanamke hupata maumivu sugu kwenye nyonga na ugonjwa wa mifupa arthritis aina ya Reiters syndrome.
Vilevile, Chlamydia huweza kusababisha ugumba kwa mwanamke kama hatapata tiba. Si hayo tu, kwa wanawake wajawazito, chlamydia husababisha wajifungue kabla ya wakati wake.
Pia mtoto anaweza kuzaliwa na maambukizi kwenye masikio, sehemu za siri, macho na kwenye mapafu yaani homa ya mapafu, na kama mtoto hatapatiwa tiba ya haraka ya macho baada ya kuzaliwa basi anaweza kuwa kipofu.
Dalili za chlamydia kwa watoto wachanga hutokea katika kipindi cha wiki mbili kwenye macho, na iwapo ni homa ya mapafu dalili zake hujitokeza katika kipindi cha wiki 2 hadi miezi 3 baada ya kuzaliwa.

JINSI YA KUJIKINGA NA UGONJWA WA ZINAA WA CHLAMYDIA.

Kwanza kabisa kama nilivyoeleza kwenye kipindi kilichopita, njia sahihi ya kujikinga na magonjwa ya zinaa ni kuacha au kuepuka kujamiiana au kufanya ngono zembe na sizizo salama.
Kwa wanawake wajawazito, ni vizuri kuhudhuria kliniki mapema wakati wa ujauzito na kupimwa vipimo mbalimbali ambapo kimojawapo ni cha kuangalia iwapo mama mjamzito ameathirika na ugonjwa huu na kupatiwa matibabu mapema.
Vile vile tumia kondomu
Kwa wale wenye maambukizi wanashauriwa kuchukua tahadhari ya kutowaambukiza wapenzi wao kwa kufanya ngono salama, pia kuepuka kushika macho kwa kutumia mikono na hata ikiwezekana kuwaepuka wapenzi wao ili kuwalinda na maambukizi.
Vilevile kwa wale ambao wapenzi wao wameambukizwa au wameonyesha dalili za ugonjwa huu, wanashauriwa na wao pia kupata tiba hata kama hawana dalili zozote.
Pia, kondomu ihusike kwa kila tendo la ngono.
Naam wasomaji, kwa hakika kama wasemavyo wahenga kinga ni bora kuliko tiba, basi tujilinde na kujiepusha na magonjwa yote  yakiwemo ya zinaa yanayoweza kuepukika,

Daima tuzilinde afya zetu!

Imeandikwa na;
Sayi manyanda
manyandahealthy@gmail.com
Credit Manyanda Healthy.
Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s