Hii hapa Hofu mpya kwa watumiaji wa simu za mkononi

Unadhani simu yako ya mkononi ni kichaka kikubwa kinachoweza kuhifadhi siri zako zote?

Jibu ni hapana. Kwani teknolojia inamwezesha mtumiaji yeyote kuingilia mawasiliano katika simu yako na kufyonza taarifa mbalimbali  kama ujumbe mfupi, barua pepe, simu zinazotoka na kuingia, picha unazopiga au kutumiwa hata video, pia inaweza kubaini eneo alipo mtu.

Kwa lugha nyepesi kitendo hiki huitwa udukuzi.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Profesa John Nkoma anafafanua udukuzi akieleza kuwa ni matumizi ya teknolojia inayowezesha kuingilia mawasiliano ya mtu katika simu au kifaa chochote cha mawasiliano.

Udukuzi wa Serikali

Novemba mwaka jana, Kampuni ya Kimataifa ya Simu za Mkononi ya Vodafone, ilitoa taarifa inayoonyesha kuwa Serikali ya Tanzania imeweka nyaya za siri katika mtandao wa Vodacom  na kunasa mawasiliano ya wateja 98,765 kwa mwaka 2013.

Katika ripoti hiyo,(Law Disclosure Enforcement), Tanzania inatajwa kuwa ni nchi ya pili duniani miongoni mwa  nchi 29 ambazo Vodafone inatoa huduma ikiwa nyuma ya Italia kwa kufuatilia, kuingilia au kunasa mawasiliano ya simu.

Italia inashika nafasi ya kwanza kwa mawasiliano 605,601 ya raia wake kufuatiliwa na taasisi za kiusalama za Serikali.

Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba alidai kushtushwa na taarifa za Serikali kunak-ili mawasiliano ya simu kwa kutumia nyaya za siri.

 “Hata mimi imenishtua kidogo kwa sababu sheria za usalama za mawasiliano, kunakili chochote kunafanyika kwa sheria tu,” anasema.

Hata hivyo, Makamba anakiri kuwa Serikali kupitia taasisi za usalama hulazimika kuomba taarifa za wateja kwa ajili ya uchunguzi.

“Wakati mwingine kutokana na vitisho vya ugaidi, kuna vitu vingine vinathibitishwa kwa njia ya kudukua mawasiliano ya simu na siyo vinginevyo,” alisema.

Makamba anasema kuwa zipo sheria zinazotoa ruhusa kwa taasisi za usalama kama Takukuru na Usalama wa Taifa kuomba mawasiliano hayo.

“Uhalifu umeongezeka sana hasa kwa kutumia simu, mara kadhaa uhalifu unafanyika kwa mawasiliano ya simu na hizo ndizo zinazotoa uthibitisho kwa hiyo ni lazima tupate uthibitisho,” anasema Makamba.

Kuhusu watu binafsi kuomba taarifa za wateja kutoka kwa kampuni ya simu, Makamba anasema kuwa mara nyingi hilo husababishwa na kuwapo kwa matatizo kati ya mtu na mtu hasa ya uhusiano.

Makamba anasema watu wamekuwa wakizitumia vibaya taasisi hizo kwani kisheria taarifa za mtu zinatakiwa kutunzwa.

Pia, kuthibiti hali hiyo, Makamba anasema, wizara yake imepeleka Muswada wa Sheria za Kulinda Taarifa za Mtu Binafsi, ambao utahalalisha namna ya mawasiliano na faragha,” anasema.

“Muswada huo umeshaandaliwa, kama mwaka huu kusingekuwa na mambo mengi kama Uchaguzi Mkuu ingeshakuwa sheria,” anasema Makamba.

Katika teknolojia hiyo, Vodafone walisema mfumo wa metadata ulitumika kunasa taarifa za wateja walengwa. “Ni rahisi kujua mambo yanayomhusu mtu, kwa mfano simu anazopiga, ujumbe mfupi, mitandao ya kijamii na picha au video anazorekodi,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.

Kadhalika, taarifa hiyo ilisema kuwa katika nchi nyingi, watu wa usalama wana haki kisheria (kulingana na sheria ya nchi) kumtaka opereta wa mawasiliano kutoa taarifa hizo za mawasiliano.

Udukuzi upo wa aina nyingi, kuna udukuzi ambao mhalifu huweza kutengeneza nambari kama za mlengwa(anayetaka kunakili mawasiliano yake) bila mhusika kujua. Kwa hiyo, simu, ujumbe mfupi vyote vitaingia kwake.

Kufanya hivyo ni kuvunja Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta Namba 3 ya Mwaka 2010 na Kanuni za Mawasiliano za kulinda wateja za mwaka 2005.

Aina nyingine za udukuzi wataalamu wa teknohama wanasema ni kwa kutumia programu maalumu inayoweza kurekodi taarifa zote za simu lengwa bila mtumiaji kujua.

Kwa mfano; ni programu ya Hellopsy au Mspy ambayo huwekwa katika simu lengwa na kunakili orodha ya namba za simu, picha unazopiga na video unazorekodi na kusikiliza simu zote mtumiaji wa simu lengwa atakazosikiliza.

Programu hizi zinaweza kuuzwa katika maduka au kwa mtaalamu yeyote wa teknohama.

Licha ya Kifungu cha 123 (1) cha Sheria ya Mawasiliano kusema kuwa; ni kosa kwa mtu yeyote ambaye bila sababu za msingi atasababisha kuingilia au kuzuia kupokewa kwa mawasiliano yoyote ya kielektroniki hapa nchini, wapo watu maarufu waliowahi kufanyiwa udukuzi.

Kwa mfano ni kawaida kuwasikia wanasiasa wakijigamba kuwa wamenakili mawasiliano kati ya mtu A na B, hivyo kujitapa wamebaini nyendo zao.

Udukuzi huo ulifanywa hata nchini Marekani, ambapo Gazeti la News of the World linalomilikiwa na bilionea Rupert Murdoch, lilifungwa kutokana na kile kinachoaminiwa kuingilia mawasiliano ya simu za watu maarufu kinyume cha taratibu.

Hapa nchini, TCRA inaeleza kuwa idadi ya watumiaji wa simu imefikia 28.2 milioni hadi kufikia Juni 2012.

Ongezeko hilo linadhihirisha kuwa teknolojia ya mawasiliano bado inakuwa kwa kasi. Pamoja na ongezeko hilo, TCRA wanasema baadhi ya nchi zina sheria ya kuingilia mawasiliano ya watu, lakini Tanzania bado hakuna sheria hiyo.

“Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya mwaka 2010 (Epoca) kifungu cha 98, kinakataza kuingilia faragha ya mawasiliano ya mtu,” anasema Profesa Nkoma.

Kadhalika kifungu cha 99 cha Epoca, kinaweka wazi masharti ya kutolewa kwa kumbukumbu za mawasiliano, iwapo zitahitajika kwenye ufuatiliaji wa masuala ya kisheria.

Profesa Nkoma anasema kuwa TCRA imeshapokea malalamiko mengi ya watu kufanyiwa udukuzi. Kwa mfano, waajiri kutumia kumbukumbu za miamala ya kifedha katika mtandao na kuzitumia kuwafukuza kazi wafanyakazi au watu kuibiwa fedha kupitia simu za mkononi.

Hatari ya simu za ‘smartphone’

Inaelezwa kuwa udukuzi hufanywa kwa urahisi zaidi katika simu za smartphone, ambazo sasa zimepata umaarufu mkubwa na zina uwezo wa kufanya mambo mengi yanayofanyika katika kompyuta.

Simu zinazoweza kuingiliwa taarifa zake ni pamoja na Android Phones, Blackberry, Windows mobile, Iphone, Ipod na Tablet.

Hata hivyo, kuna simu ambazo zimeundwa na mfumo wa kurekodi simu unazopokea au kupiga bila wewe kujua.

Simu hizo hurekodiwa na kuhifadhiwa katika kasha (folder) maalumu.

Kwa kawaida ni rahisi kulifikia kasha hilo kama uwezavyo kufikia ujumbe mfupi. Njia hii ni nyepesi kwa waingiliaji wa simu yako kuchukua kasha hilo na kusikiliza simu zako kwa urahisi.

Utajuaje?

Namna ya kujua kuwa simu yako ya smartphone imeingiliwa, mlio kama wa mtetemo (vibration) hutokea mwanzoni kabisa wakati unapiga simu au wakati unapokea.

Wataalamu wa teknohama wanasema kuwa wamejaribu kufuatilia simu zenye programu hiyo na kubaini kuwa ni watumiaji wa simu za bei nafuu ambazo zimepata umaarufu zaidi nchini kuwa ndizo zinaweza kuingiliwa kimawasiliano.

Wakati huohuo utafiti wa Shirika la Takwimu za Kiuchumi la Kimataifa (IDC) unaeleza kuwa zaidi ya simu 22 milioni aina ya smartphone zinatarajiwa kuuzwa barani Afrika ifikapo mwaka 2015.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Simu za Smartphone, aina ya Huaiwei, Tawi la Tanzania, Bruce Zhanga anasema, kwa sasa watumiaji wa simu hizo ni asilimia 15 ya Watanzania wote.

Anasema kuwa kampuni hiyo imeshusha bei ya simu hizo hadi kufikia 160,000, ili kuhakikisha kila mmoja hata waishio vijijini wanapata aina hiyo ya simu.

Dakika tano tu zitakuwezesha kuingilia taarifa za simu lengwa.

Mara tu unapoiweka programu hii katika simu lengwa (yaani ya yule unayetaka kumfuatilia) baada ya dakika tano utaweza kuanza kupata taarifa zake.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited, Sebastian Nkoha anasema vitendo vya uingiliaji wa mawasiliano vinasababishwa na kukua kwa teknolojia.

Akizungumzia namna mawasiliano yanavyoingiliwa, Nkoha anasema mtu anaweza kupata programu wakati wowote katika kompyuta na kuiweka katika simu lengwa kabla ya kuanza kuingilia mawasiliano hayo.

“Teknolojia imekua na imefikia mahali hata wanandoa wanaingilia mawasiliano kwa ajili ya kunakili taarifa za wenza wao,” anasema.

Anasema njia kubwa ambayo inaweza kutumiwa na wengi ni kwa kutumia ‘bluetooth’ kwa mfano ipo programu iitwayo Super Bluetooth Hack ambayo inaweza kuingilia simu zenye bluetooth.

“Kwa wale ambao wanaacha bluetooth zao wazi, ni rahisi mtu akakutumia faili na endapo utalipokea kupitia simu yako, anaweza kudhibiti mawasiliano yako yote, kwa kutumia programu iitwayo kitaalamu, ‘super bluetooth hack’,” anasema Nkoha.

Licha ya simu, pia wataalamu wa teknohama wanasema, unaweza kuingilia mawasiliano ya facebook, barua pepe hata, wi-fi na hata nywila (password) ya mtu mwingine.

Credit Mwananchi.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s