Mauaji ya Polisi Ikwiriri, Yadaiwa kuna kundi linakusanya silaha kwa uasi huku Al-shabab watajwa

MAZITO yameibuka kufuatia tukio la majambazi kuvamia Kituo cha Polisi Ikwiriri, Rufiji, Pwani na kuwaua askari wawili kisha kuchukua bunduki 7, risasi 60 na mabomu kadhaa, Uwazi limeichimba.Tukio hilo lililozua hofu ndani ya Jeshi la Polisi Tanzania, lilijiri Januari 21, mwaka huu na hadi wakati tunaenda mitamboni, hakuna mtuhumiwa anayeshikiliwa.

Ndugu wa karibu wa marehemu, Judith Timothy (32) wakilia kwa uchungu.

Askari waliouawa katika kituo hicho ni Edger Jerald Mlinga (43) na Judith Timothy (32). Afande wa tatu alifanikiwa kukimbia na hivyo kuokoa maisha yake.

UWAZI LAANZA KUCHIMBA

Muda mfupi baada ya kutokea kwa tukio hilo, timu ya waandishi wa gazeti hili ilitua katika eneo la tukio na kushuhudia damu ya askari hao waliouawa kwa kukatwa mapanga, Judith licha ya kukatwa alipigwa risasi tumboni.

MAJIRANI WAONGEA NA UWAZI

Baadhi ya wananchi wanaoishi jirani na kituo hicho walizungumza na Uwazi na kusema kile walichokiona.“Mimi muda wa tukio nilisikia kelele za kuomba msaada kutoka kwenye kituo hicho. Nilijua kuna watuhumiwa wanabanwa na askari maana kelele hazikuwa za mtu mmoja kulikuwa na ya kike pia.

“Lakini nilipozidi kusikiliza kwa umakini nilibaini kuwa, kelele hizo zilikuwa za kuomba msaada kwani walikuwa wakishambuliwa na wakawa wanapiga mayowe, ‘tunauawa’,” alisema mkazi mmoja wa Ikwiriri huku akiomba hifadhi ya jina lake.

WANANCHI WATOKA, MLIO WA RISASI WASIKIKA

Wakiendelea kuzungumza, majirani hao walisema walijikuta wakijikusanya kwa ajili ya kwenda kituoni hapo kujua kulikoni lakini ghafla walisikia mlio wa risasi hivyo wakarudi ndani mbio na kujifungia.“Baadaye sana sikusikia tena mlio wa risasi wala mayowe ya kuomba msaada. Mimi nilitoka kwenda kituoni, nikashangaa kukuta watu wengi wamesimama nje.

Nilipofika nikaambiwa kituo kilivamiwa na majambazi, wamewaua askari wawili. Kweli, maana miili yao ilikuwa chini kwenye dimbwi kubwa la damu. Nilishtuka sana kwani kama askari wenye silaha wanavamiwa na majambazi je sisi raia tusio na silaha?” alihoji jirani huyo.

ASKARI WA KIKE ALIPONZWA NA SIMU

Habari zaidi zinasema kuwa, marehemu Judith yeye aliponzwa na simu yake ya mkononi.
Yule afande mwanamke alishamaliza kazi akaondoka, lakini alipofika mbele akienda  nyumbani akagundua amesahau simu, ikabidi arudi.“Kule kurudi ndiyo na majambazi nao wakatokea,” alisema afande mmoja kwa ombi la kutotaja jina lake gazetini.

UTENDAJI WA KAZI ULIKIUKWA?

Taarifa kutoka chanzo chetu ndani ya jeshi la polisi zinadai kuwa siku ya tukio kituoni hapo kulikuwa na polisi watatu, wawili walipaswa kuwepo kaunta ndani, mmoja awepo nje.Hata hivyo, wote walikuwa nje na ndipo ghafla wakavamiwa na kundi hilo la watu wasiopungua kumi nao wakashindwa kujitetea na kujikuta wawili wakiuawa.

UGAIDI WATAJWA

Huu ni ugaidi kabisa! Haiwezekani kituo kikatekwa kirahisi na askari kuuawa. Hawa watu wanaovamia vituo vya polisi na kuchukua silaha wanazipeleka wapi? Niliwahi kusikia kuwa kuna kundi la watu ndiyo wanaoteka vituo na kupora silaha kwa lengo la kukusanya silaha.“Nasikia hao watu iko siku huko mbele watakuja kufanya uasi mkubwa sana hapa Tanzania,” alisema jirani mwingine.

AL SHABAAB WATAJWA

Habari zaidi kutoka kwa vyanzo vya kiserikali zinasema kuwa, upo wasiwasi wa kundi la Al Shabaab kutumia nafasi hiyo kukusanya silaha ili baadaye wawape vijana ambao wamekuwa wakipewa mafunzo na kundi hilo.

Habari zikakumbushia kuwa, Julai mwaka 2013, mkoani Mtwara kuna vijana 11 walikamatwa wakiwa na CD 25 zenye mafunzo ya wapiganaji wa Al Shabaab na Al Qaeda.“Serikali lazima iliangalie hili. Silaha zinatekwa, hadi mabomu yanachukuliwa na majambazi, wanapeleka wapi? Mbona hatusikii matumizi makubwa ya mabomu sehemu mbalimba za nchi? Ni majambazi kweli au makundi ya Al Shabaab?” alihoji mtoa hoja hii akiomba kufichwa kwa jina lake.

MKE WA MAREHEMU MLINGA

Baada ya kuzungumza na majirani, Uwazi ilikwenda Hospitali ya Mkuranga, Pwani ambako miili ya marehemu ilihifadhiwa na kuzungumza na ndugu. Kwa upande wake, mke wa marehemu Afande Mlinga, Walivyo Ahamed Wapiwapi alisema kifo cha mumewe kimempa mshtuko mkubwa kiasi kwamba hajajua ataishije na watoto wanne aliowaacha.

Nakumbuka saa moja na nusu siku moja kabla ya tukio mume wangu alirudi kutoka kazini, alikaa kidogo, ilipofika saa tatu akaaga kwamba anakwenda kazini.“Siku hiyo hakurudi tena mpaka kesho yake saa nne asubuhi napigiwa simu na mashemeji zangu kwamba mume wangu ameuawa kituoni,” alisema mwanamke huyo huku akimwaga machozi.Kwa mujibu wa ndugu wa marehemu, mwili wake ulisafirishwa juzi na ulitarajiwa kuzikwa jana Jumatatu kwenye Kijiji cha Mbokomu, Kilimanjaro.

MDOGO WA MAREHEMU JUDITH

Naye mdogo wa marehemu Judith, Oscar Mwambije alisema:
Mimi taarifa za kuuawa kwa dada nilizipata usiku uleule kutoka kwa kaka anayeishi Mwanza ambaye ndiyo wa kwanza kupata habari hizo.“Aliniambia Judith amepigwa risasi kazini na kufariki dunia palepale na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi.

Tulikuja hadi hapa chumba cha kuhifadhia maiti Mkuranga tukakuta akishushwa katika gari la polisi na tulithibitisha kuwa ndiyo yeye dada Judith,” alisema mdogo wa marehemu huku akilengwalengwa na machozi.Kwa mujibu wa familia, marehemu Judith amezikwa Ijumaa iliyopita kwenye Kijiji cha Itete wilayani Rungwe, Mbeya. Ameacha mtoto mmoja.

MAELEZO YA KAMANDA

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, SACP Ulrich Matei akiwa Mkuranga na waandishi wetu alisema: “Msako mkali sana unaendelea, lazima wahusika wapatikane.

MKURUGENZI MAKOSA YA JINAI

Kaimu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Tanzania (DCI), Kamishna Diwani Athuman alipohojiwa na Uwazi kuhusiana na tukio hilo kutokana na madai ya wananchi kwamba kuna kundi la watu linakusanya silaha na baadaye kuanzisha vurugu au vita nchini, alisema:

Wanaofanya uhalifu wana sababu zao, hao pia wana sababu zao, kwa namna gani watatumia hizo silaha, hatujui ila msako mkali wa kuwatafuta unaendelea na ninawaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi ili kuwatia nguvuni watu hao,” alisema Kamanda Athuman.

KUMBUKUMBU ZA NYUMA

Kuvamiwa kwa Kituo cha Polisi Ikwiriri kumekuja mara baada ya vituo vingine navyo kuvamiwa, kuibwa silaha na polisi kuuawa.Kituo cha Polisi Bukombe, Geita Septemba, mwaka jana, saa tisa usiku kilivamiwa ambapo askari wawili waliuawa na bunduki 10 na mabomu kuporwa.Mwaka huohuo, Kituo cha Polisi Kimanzichana, Mkuranga, Pwani nacho kilivamiwa na majambazi. Polisi mmoja aliuawa na mwingine kujeruhiwa, bunduki tatu ziliibwa.

Credit GPL

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s