Haya ndiyo maneno ya mwisho yule Polisi aliyeuawa akimuokoa mtoto

KILA nafsi itaonja mauti! Maneno ya mwisho ya Koplo Joseph Isaac Swai (27) aliyeuawa kwa kucharangwa mapanga na Tisi Sirili Mallya (29) katika zoezi la kumwokoa mtoto Valerian Tisi (miezi nane) asichinjwe, yanazidi kuzua simanzi, Uwazi limenasa mkononi.

Katikati ya wiki iliyopita, eneo la Chang’ombe mjini hapa, Koplo Swai aliyekuwa akitumia namba ya uajiri wa polisi G. 7168 alikatwakatwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili na Mallya kisa ni afande huyo kwenda nyumbani kwa mtuhumiwa huyo na kumtaka asimuue  mwanaye ambaye alikuwa katika hatua za mwisho za kumchinja akiwa amemning’iniza.

YA SIKU TATU KABLA

Akizungumza na Uwazi kwenye msiba wa Koplo Swai mjini hapa, rafiki mmoja wa karibu huku akiomba jina lake lisitajwe gazetini kwa sababu yeye si msemaji wa familia, alisema:

“Bado naumia sana, unajua siku tatu kabla ya hili tukio, marehemu aliniambia hajisikii sawasawa. Nilimuuliza kama anaumwa akasema hapana, ana matatizo ya kifedha akasema si sababu, ila hajielewielewi tu.

Mimi nilijua ni hali ya mwili, kuna wakati unakuwa mzito wakati mwingine mwepesi lakini baada ya kuuawa sasa  ndiyo nimejua kwa nini afande Swai alikuwa akisema hajisikii sawasawa.

ALISEMA AMEWAMISI NDUGU ZAKE

Rafiki huyo alisema siku ya tukio, muda mchache, Swai alimpigia simu na kumwambia anatamani kwenda kwao (Kilimanjaro) kusalimia ndugu zake, anahisi kuwamisi sana. Pia aliniambia alikuwa studio moja ya redio mjini Dodoma (Dodoma FM Radio) ndiyo amerejea.”

AKATA SIMU BAADA YA KUITWA

Akizungumzia namna tukio la afande huyo kukatwakatwa mapanga hadi kifo, rafiki huyo ambaye naye ni polisi, alisema:

Wakati tukizungumza kwa simu, ghafla akasema atanipigia baadaye kuna mtu anapiga simu. Sikuwa na maswali juu ya hilo wala sikushtuka mpaka nilipokuja kusikia kuwa, amekumbwa na mauti kwa njia hiyo ya kikatili.

ALICHOELEZEWA RAFIKI HUYO

Kwa mujibu wa rafiki huyo, Swai alipigiwa simu na Mtendaji wa Mtaa wa Chang’ombe, Oliver Balthazar akimwambia kuna mzazi (Mallya) anamtesa mwanaye na huenda angemuua kwani tayari alishamning’iniza kichwa chini na panga liko mkononi.“Niliambiwa mtendaji huyo alimpigia Swai akiamini ni polisi hivyo angeweza kunusuru uhai wa mtoto huyo ambaye alikuwa akilia kwa sauti ya juu.”

ALIGOMA KWENDA

Ilizidi kudaiwa kuwa, baada ya afande huyo kuambiwa taarifa za baba kutaka kumchinja mwanaye, aligoma akisema, ‘siwezi kwenda, siku hizi raia wanaua sana polisi.’
Baada ya sekunde kadhaa, inadaiwa Swai akasema: “Oke, poa nitakwenda maana ni majukumu yangu.”

ALIONGOZANA NA WATU WAWILI

Afande Swali alitoka nyumbani kwake mpaka kwenye ofisi ya mtendaji huyo na kutoka naye. Aliongozana na mtendaji na mtu mwingine ambaye anashughulika na kitengo cha kuhudumia watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

Njiani, habari zinasema, afande Swai alikuwa akishangaa ni baba wa aina gani mwenye dhamira ya kumshika mtoto wake na kumtesa na kutoa kauli za kumchinja. Inadaiwa alisema:
 “Hivi huyo baba ni mzima kweli? Mwanao wa kumzaa umtese, useme utamchinja! Kwa kosa gani kubwa?

HALI YA NYUMBANI KWA MTUHUMIWA

Ikaendelea kuelezwa kwamba, Koplo Swai alipofika nyumbani hapo alimkuta Mallya bado anamtesa mtoto wake na safari hii mtoto alikuwa halii tena.

Inaelezwa kuwa, Swai aligonga mlango na kujitambulisha lakini mtuhumiwa alipofungua mlango alionekana amemning’iniza mtoto wake kichwa chini, miguu juu huku akisema anamchinja.
Swai alimsihi Mallya kuachia panga chini akitumia lugha ya upendo lakini Mallya akasema lazima amchinje. Ndipo Swai akawa anamsogelea lengo lake lilikuwa ni kumrukia mtuhumiwa huyo kwa kumkumbatia ili amnyang’aye panga.

KAMA SI MGUU WA KUSHOTO

“Wakati anamsogelea, Swai alipanua mikono tayari kwa kumrukia na kumkumbatia. Lakini mikono ikiwa bado hewani, mguu wa kushoto uliteleza hivyo safari ya kumfikia Mallya ikaishia hapo, maskini jamaa akaenda chini.
Pengine kwa hasira  za kuona afande huyo alitaka kuingilia dhamira yake, Mallya alimtupa mtoto chini na kuanza kumcharanga mapanga koplo huyo,” kilisema chanzo kingine.

ALIPIGA MAGOTI ASIUAWE

Habari nyingine zinasema, wakati Mallya ameshapeleka mapanga mwilini, Swai alipiga magoti na kuomba asimuue kwa vile alikuwa ana mipango ya ndoa (haikufafanuliwa), lakini mtuhumiwa huyo hakumsikiliza.

MTENDAJI, YULE MTU MWINGINE

Inaelezwa kwamba, baada ya kuona Mallya anamcharanga mapanga Swai bila huruma, yule mtendaji na yule mtu mwingine aliyekuwa naye walitimua mbio mbali huku wakianza kupiga kelele za kuomba msaada.

MAMA AMKWAPUA MTOTO

Huku Mallya akizidi kumcharanga mapanga afande huyo, mama wa mtoto alimkwapua mwanaye aliyekuwa chini na kukimbia naye ambapo mpaka sasa amefichwa kusikojulikana.

MAVAZI SIKU YA MAUAJI

Siku hiyo, Mallya ambaye ni maji ya kunde alivaa suruali ya ‘jinsi’ rangi ya bluu, fulana rangi ya bluu iliyoiva na kapelo nyeupe.

KUHUSU MTUHUMIWA

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, SACP David Misime, mtuhumiwa Mallya aliuawa na wananchi wenye hasira kali usiku wa Jumatano iliyopita, saa tano akiwa na panga alilofanyia mauaji ya afande huyo.

Kamanda Misime alisema baada ya Mallya kutekeleza mauaji hayo alikimbilia mafichoni, lakini ilipofika saa tano raia  walimuona maeneo ya Mtimkavu Maili Mbili akiwa  na panga alilotumia kumuua Koplo Joseph huku nguo zake zikiwa zimetapakaa damu.

KUMBUKUMBU MBAYA

Kamanda Misime alisema katika kumbukumbu za kipolisi, mwaka 2006, Mallya alifungwa miaka mitatu jela kwa kosa la kujeruhi. Mwaka 2009 alifungwa tena, miezi sita kwa kosa la kutishia kuua.

SWAI AZIKWA

Mwili wa marehemu Swali ulisafirishwa kwao Moshi, Kilimanjaro, Februari 5 na mazishi kufanyika Februari 7, mwaka huu. Mungu ailaze pema peponi, roho ya marehemu. Amina.

Credit GPL

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s