Mambo 5 yanayoleta uadui kwa wapenzi!

Rafiki, bila shaka ipo wazi kwamba kila mmoja anapenda kuwa na mpenzi ambaye mbali na kumpenda kwa moyo wake wote, atapenda kumfanya awe kama ndugu, rafiki au zaidi ya hapo. Atakayekuwa tulizo la moyo, kivuli kwenye jua kali, maji jangwani na tiba kwenye maradhi.

Hakuna anayeweza kuukabidhi moyo wake kwa mtu ambaye anajua fika kwamba atamtesa, atamnyanyasa, kumsababishia maumivu ya moyo, kuwa kero kwenye maisha yake na ‘kum-treat’ kama adui yake.

Mapenzi ni sanaa kama zilivyo sanaa nyingine. Kwa mfano, ili kumudu kupiga gitaa au kinanda na kupata muziki mzuri, ni lazima ujifunze. Kwenye mapenzi ni hivyohivyo, ili kuishi vizuri na mpenzi wako ni lazima ujifunze. Usichoke kujifunza kila kukicha ili kuwa na uhusiano imara na ndoa inayoweza kudumu, jifunze kupenda na kumuenzi umpendaye kwa moyo wako wote.

Labda nikuulize rafiki yangu, wewe ulijifunzia wapi mapenzi? Shuleni, nyumbani, chuoni, mitaani au mtandaoni? Yawezekana ukatafsiri mapenzi kwa maana ya tendo la ndoa lakini hapa simaanishi hivyo, nazungumzia sanaa nzima ya mapenzi katika tafsiri pana.

Ukweli ambao unashangaza, watu wengi wana uelewa mdogo juu ya suala zima la maisha ya kimapenzi, jambo ambalo linasababisha waishi kimazoea na kushindwa kufuata misingi halisi ya jambo hilo nyeti katika maisha.

Matokeo yake, watu ambao awali wakati wanaanzisha uhusiano wa kimapenzi walikuwa wanapendana na kugandana kama ruba, huishia kuwa maadui na kuvunja uhusiano wao kwa majuto mengi. Yaani mtu ambaye awali alikuwa kipenzi cha roho yako, anabadilika na kuwa mwiba mkali maishani mwako.

NINI HUMFANYA MPENZI AWE ADUI?

Kwa kawaida, mnapoanzisha uhusiano wa kimapenzi kila mmoja humueleza au kumuonesha mwenzake nini anapenda na kipi hakimfurahishi. Kwa kuwa mapenzi ni suala la hiyari, mwenzio anapokukabidhi moyo wake anategemea kuwa utayafanya yale yanayomfurahisha na kuepuka yale yanayomuudhi kwa kadiri uwezavyo. Wataalam wa mapenzi wana msemo mmoja kwamba ‘penzi la kweli humsukuma mtu kumfurahisha mpenzi wake kwa kadiri ya uwezo wake na kamwe halitafuti visingizio’.

Usitafute visingizio linapokuja suala la kumfurahisha mwenzio. Yafuatayo ni baadhi ya mambo ambayo yanaweza kumgeuza mpenzi wako akawa adui yako.

1.UKISHINDWA KUMSIKILIZA

Mapenzi ni kusikilizana kwa kila jambo, hakuna nguzo muhimu kama kukubali kuupokea udhaifu wa mwenzako. Jenga mazoea ya kumsikiliza mpenzi wako kwa staha! Hata kama amekukwaza (lazima itatokea tu kwani yeye siyo malaika), tafuta namna nzuri ya kufikisha hisia zako kwake.

Kabla ya kumsikiliza usikimbilie kumhukumu, kumsimanga, kumvunja moyo au kutoa kashfa ambazo zitamfanya asononeke ndani ya moyo wake kwani vitu hivyo vikizidi, hupunguza hisia za upendo na chuki huanza kujengeka taratibu.

2. MAUDHI YA MARA KWA MARA

Wachambuzi wa masuala ya mapenzi, wanaeleza kwamba miongoni mwa sumu ambazo zinaweza kumgeuza mwenzi wako na kuwa adui yako ni kitendo cha kumfanyia maudhi yanayojirudia.
Kama unataka kuishi kwenye uhusiano wenye amani, epuka maudhi ya mara kwa mara kwa mwenzako. Endapo ameshakwambia kwamba jambo fulani halipendi, msikilize na muoneshe kwa vitendo kwamba umebadilika.

3. KUFOKEANA MBELE ZA WATU

Yawezekana amekuudhi kiasi kwamba umeshindwa kuzidhibiti hasira zako, matokeo yake unaanza kumpandishia au kumfokea mbele za marafiki zake, ndugu au watoto. Jambo hili hujenga chuki kali ndani ya moyo wa anayetendewa na taratibu ataanza kukutoa thamani.
Hata kama umechukia kiasi gani, kamwe usimfokee mwenzako mbele za watu, tafuta muda ambao utakuwa umetulia, zungumza naye kwa upole na bila shaka mtafikia muafaka wa kilichokuwa kimekukasirisha.

4. KUSHINDWA KUHESHIMU NDUGU ZAKE

Familia zetu za Kiafrika, tuna kawaida ya kutembeleana mara kwa mara, yaani kama ni mume, ndugu wa mke watakuja nyumbani kwenu na kama ni mke, ndugu wa mume watakuja nyumbani kwenu.
Hakuna jambo baya kama kuonesha chuki kwa ndugu wa mwenzako, hii itamfanya mwenzako aamini kwamba mapenzi yako kwake ni ya msimu. Taratibu ataanza kukushusha thamani.

5. KUKOSA UAMINIFU

Jambo kubwa ambalo ndiyo mhimili wa uhusiano wowote wa kimapenzi ni uaminifu kwa mwenzi wako. Mapenzi ya kweli yanajengwa na uaminifu, kamwe usithubutu kuuchezea kamari moyo wa mwenzako. Yaani yeye anakupenda na kukupa heshima zote unazostahili lakini nyuma ya pazia, unachepuka na mwingine.
Hata kama alikuwa anakupenda vipi, akigundua upendo utabadilika na kuwa chuki kali ndani ya moyo wake ambayo itadumu kwenye moyo wake. Jitahidi kumfanyia mambo mazuri na kamwe usiuumize moyo wake.
Advertisements

Je, unazijua sifa za mwanaume anayefaa kuwa mwenza wako?

Je, unazijua sifa za mwanaume anayekufaa kuwa mwenza wako? Hili limekuwa swali gumu kwa wanawake wengi ambao wamekuwa wakijiuliza watawezaje kuwafahamu au kumfahamu mwanaume f’lani kama ana sifa za kuwa mpenzi wake? Mwanaume anayekufaa katika uhusiano wa kimapenzi lazima awe na sifa zifuatazo;

AWE CHAGUO LAKO

Ni lazima mwanaume unayetaka au unayempenda awe mpenzi wako, awe na sifa kubwa ya wewe mwenyewe kumpenda, kumridhia na siyo kumpenda kwa sababu au shinikizo f’lani.

MWENYE KUJIAMINI

Mwanamke anapokuwa na mwanaume anayejiamini, anaamini yupo salama zaidi. Hata kama kuna lolote linaloweza kutokea wakiwa wote basi mwanamke hatakuwa na woga kwa sababu tu anaamini yupo na mwanaume mwenye kujiamini ambaye atakuwa kinga au mtetezi wake.

MWENYE UAMUZI

Mwanaume mwenye uamuzi ndiye anayekufaa kwa ajili ya kujenga uhusiano makini na ulio bora. Yule mwenye uwezo wa kusema jambo na kulisimamia. Awe mtu mwenye msimamo na asiyetetereka kwa jambo lolote linaloweza kumyumbisha katika uhusiano wake, kwa sababu yeye ndiye aliyeamua kupenda basi hayuko tayari kusikiliza maneno ya pembeni kwa sababu anaamini katika fikra zake.

ASIWE MVIVU

Ili kuhakikisha kuwa familia au uhusiano wako hauyumbi, mwanaume asiyekuwa mvivu ndiye anayekufaa.

Awe mtu ambaye anajituma ili kudumisha penzi na hata familia yake. Uvivu ninaouzungumzia hapa ni ule wa kimajukumu ya kutafuta fedha na anapokuwa faragha.
shutterstock-couple-huggingANAYETUNZA SIRI

Katika uhusiano wako kuwa na mwanaume mwenye uwezo wa kutunza siri za ndani hata kama mtakuwa mmekoseana au kuhitilafiana. Awe tayari kuvumilia jambo hilo moyoni mwake. Kama ukiona amelitoa nje basi ujue limemzidi uwezo, ndiyo maana kuna wakati mtu akitaka kukwambia jambo anakuuliza ‘je, una kifua?’

Kuna mambo mengi sana nyuma ya uhusiano ambayo mengine hayastahili kumwambia kila mtu hivyo lazima mwanaume wako awe mtunza siri.

ASIYEPAYUKA

Uhusiano wowote una migongano kama ambavyo kazi zote zina changamoto katika utendaji wake. Kwenye uhusiano, unapaswa uchague mwanaume asiye na tabia ya kupayuka mnapokuwa mmekosana. Tabia ya kupayuka kiasi cha kuwafanya hata majirani wajue jambo mnalogombania haifai.

Ulishajiuliza unapenda nini kwa mpenzi wako?

Leo kwenye safu hii nimekuja tuongelee suala hili la wapenzi kupendana na kufikia kuwa mwili mmoja je, umewahi kujiuliza maswali kuhusiana na mwenza wako? Maswali haya yanawahusu wote.

Mnatafuta nini ndani ya wenza wenu ni kitu gani mnaangalia/mnakiona ndani ya mtu unayeamua kuwa naye kama mchumba/mume/mke. Je, ni macho yake au tabasamu, ama ni muonekano wake, uchangamfu au upole, ni kitu gani unachokiona ndani ya mtu kinachokuvutia. Wengine wanavutiwa jinsi mtu anavyofikiria, au mwili wake, wewe je?

Unaweza ukawa umevutiwa na kitu kimojawapo, lakini unajua uhusiano mzuri haujengwi na vitu hivi tu, kuwa na uhusiano mzuri na mwenza wako inahusisha vitu vingi sana tofauti na tabasamu lake iwe unatafuta mtu wa kuwa naye au kama tayari upo katika uhusiano hakikisha mnakubaliana vitu muhimu ambavyo mkividharau kisa umempenda kwa sababu ya shepu yake au ucheshi wake vinaweza kuharibu uhusiano huko mbele ambapo ni pagumu zaidi.

Vitu unavyotakiwa kuangalia zaidi

Hivi ni baadhi ya vitu unavyotakiwa kuangalia ndani ya mwenza wako kama unataka uhusiano mzuri na kama kweli atakuwa mke au mume, epuka kuangalia vitu vya awali kama hivyo nilivyovitaja hapo.

Anakupa heshima yako, haijalishi kama yeye ni mkubwa kwako, na hapa heshima siyo salamu kama wengi mnavyodhani.

Anaheshimu maamuzi yako, kama ni katika kazi au kitu unachoamua kufanya na siyo kukucheka au kukudharau.

Hakukatishi tamaa anakuunga mkono kwenye kila jambo na kukupa moyo wa kushinda kila wakati.
Hakasiriki ukijipa muda na marafiki au familia yako, unatakiwa kuwa na uhuru wa kujichanganya na watu wengine siyo yeye tu.

Anasikiliza mawazo yako na kukushauri

Mnashea vitu unavyovipenda kama vile kuangalia muvi, aina ya muziki, kucheza. Angalau muwe na kitu kimoja ambacho wote mnapenda ili muwe na kitu cha kufanya pamoja, vitu vingine mnaweza kutofa-utiana haina shida kwa sababu hata mapacha waliozaliwa pamoja kuna wakati huwa wanato-fautiana lakini iwe kuna kitu mnaendana ambacho mtashiriki pamoja.

Mpenzi huyo asiwe mkaidi kwa kila kitu unachomwambia, hii inawahusu wapenzi wote si wanaume ama wanawake tu.

Awe anaheshimu mipaka yako, siyo atake kujua kila kitu chako kama vile kukagua simu au wapi unapokuwa saa 24, kama mpo katika uhusiano mnatakiwa mheshimiane maana mwanzo wa kufuatiliana saa zote ndiyo mwanzo wa ugomvi usiyoisha.

Asiogope kukuambia anavyojihisi, hii itawasaidia hata pale mtakapokuwa na matatizo ili muweze kusuluhisha mambo yenu, itawaondoa kwenye hali ya kila mtu kumuwekea mwenzake kinyongo.

Kumbuka uhusiano unahusisha watu wawili, wewe na patna wako muwe na usemi ndani ya uhusiano wenu na msiogope kuambiana mnachohisi na kusikilizana pia.

Ndani ya kila uhusiano kuna kugombana, hiki ni kitu cha kawaida kabisa. Wale mnaowaona wana furaha katika uhusiano wao wameweza kujua jinsi ya kuyamaliza matatizo yao.

Usimpende mtu kwa sura, fedha, uvaaji wake bali iwe kwa mapenzi ya dhati.

Unapofeli kufanya ‘rehearsal’ ya ndoa, tegemea maumivu!

Leo tunakwenda kuitazama mada iliyopo mezani. Ndugu zangu, kama ingekuwa ni mtihani basi tunaweza kusema hakuna mtihani mgumu kufaulu kama wa kumpata mwenza sahihi wa maisha. Wengi sana wamefeli, najua wewe pia ni shahidi katika hili.

Kwa kudhamiria au kutodhamiria, wengi hujikuta wameingia kwenye ndoa na mtu ambaye si sahihi. Ukifanya utafiti kwa sasa, watu waliofunga ndoa miaka kumi au zaidi iliyopita, utagundua kati ya wanandoa kumi, wanne au watano pekee ndiyo watakuwa wanafuraha na amani katika ndoa zao.

Wawe na muda mfupi au mrefu tangu waingie kwenye ndoa, wanachokishuhudia kwa sasa ni tofauti na matarajio waliyokuwa nayo. Hii inatokana na nini? Wapendanao wengi wanapokuwa kwenye uchumba, huwa hawatumii  vizuri nafasi hiyo kufanya ‘rehearsal’.

Kwa kawaida, kuna ‘vimitihani’ vidogovidogo vingi huwa wapendanao wanapitia lakini  kwa namna moja au nyingine wanakuwa wakivipotezea. Mtu anaamini mpenzi wake ni rahisi kubadilika mbele ya safari hivyo kumpa nafasi ya kuzidi kushibana.

Wengine kutokana na kuzidiwa na nguvu ya mapenzi, hawana muda wa kuangalia hivyo vimitihani. Wanaongozwa na matamanio. Wengine wanaongozwa na tamaa ya vitu kama fedha na mambo mengine.

Wanavifuga vimitihani kwa muda mrefu katika kipindi cha uchumba pasipo kujua ni jipu. Hawafikirii kabisa kwamba vimitihani hivyo vinaweza kuwa na madhara makubwa sana vitakakuwa jipu na kutumbuka wakati wakiwa tayari wameyaanza maisha ya ndoa.

Hapa nazungumzia zaidi tabia, nidhamu, uvumilivu na hulka mbalimbali. Japo kuna vitu mtu anaweza kuvificha katika wakati wa uchumba lakini Waswahili wanasema nyota njema huonekana asubuhi. Ni rahisi sana kumjua mtu kama anafaa au hafai.

Kwenye safari ya uchumba, kama umeona mwenzako ana tatizo la ulevi uliopindukia. Akishalewa anakuwa mkorofi, anaweza kukushikia panga muda wowote, ‘rehearsal’ yako ni kumueleza madhara na kumpa muda wa kubadilika kisha umpime kama amebadilika au laa!

Usikubali kumuacha hivyo alivyo ukategemea aje kubadilika wakati tayari mmeshaingia kwenye ndoa. Akiingia ndiyo itakuwa balaa zaidi. Kama alikuwa kwenye uchumba alikuwa  anakukosakosa kukukata, anaweza kuja kukukata kabisa mkiwa ndani ya ndoa. Hakikisha hulka hiyo unaitibu, ukishindwa usiendelee mbele.

Ukikubali kuingia kwenye ndoa katika hali hiyo, tegemea maumivu huko mbele ya safari. Kama mwenzako ni malaya, hatulii nyumbani, rehearsal yako ni suala la kumbadilisha aachane na hiyo tabia. Mueleze kwa kirefu madhara ya tabia hiyo na umpe muda wa kubadilika, asipofanya hivyo, achana naye mapema.

Mpime kuhusu uvumilivu. Kama anaweza kukupenda katika nyakati zote. Uwe kwenye shida au raha. Mpime katika nyakati ngumu. Ikiwezekana mtengenezee mazingira magumu, mpime kuhusu uwezo wake wa kukabiliana na magumu.

Kwenye kipindi kama hicho, watu huweza kukimbiana. Unapompa mazingira magumu, akayaona hayawezi ni rahisi kukukimbia. Atamfuata mwingine ambaye hana mazingira magumu. Akifanya hivyo utakuwa umeshapata jibu.

Nasema hayo kwa sababu uzoefu unaonesha. Wengi hukurupuka katika ndoa. Hawajiridhishi vya kutosha katika hatua za awali. Matokeo yake wanaishia kukutana na maumivu mbele ya safari. Hapo ndipo wanajuta, wanatamani kuzirudisha siku nyuma ili watengue ndoa lakini wanakuwa wamechelewa.

Ukitegemea kupata kitu penzi utaliona chungu

Si jambo la kushangaza kuwaona au kusikia mwanamke na mwanaume wanapendana. Yaani kila mmoja anampenda mwenzake na hivyo kuanzisha uhusiano.

Hapa nazungumzia upendo wa umoja na si wa wingi. Yaani wale wanaopendana huku kila mmoja akiwa hana mwenza mwingine. Inapotokea mtu ana mwenza halafu akapenda kwingine, huo ni usaliti na si mada yangu ilipolalia wiki hii.

MADA YENYEWE

Mada yangu inajieleza hapo juu; ukitegemea kitu penzi utaliona chungu.
Wapo watu ambao wanaingia kwenye mapenzi kwa sababu ya kupenda kutoka kwenye sakafu ya mioyo yao. Yaani mfano, mwanamke anatokea kumpenda mwanaume fulani pasipo na sababu yoyote. Huo ndiyo upendo unaoitwa wa dhati!

Lakini wapo wanaopenda kwa sababu ya kitu. Mfano, mwanamke anatokea kumpenda mwanaume kwa sababu ana gari, ni msomi, ana pesa,  ni mfanyabiashara, ana cheo serikalini, ni staa wa mpira wa miguu, ni mwimbaji mzuri wa Bongo Fleva au ana umaarufu sana mitaani.

HATA MBWEMBWE ZINA UPENDO?

Katika hili, nimewahi kushuhudia dereva wa bodaboda akipendwa na msichana kwa sababu tu ya uendeshaji wake wa bodaboda mitaani. Akiingia watu wanajua huyo ni Yusuf kwani mlio mkubwa, mwendo kasi akiwakwepa watoto wa mitaani, honi nyingi, breki za ghafla, sehemu nyembamba anapita kwa spidi na watu wanamsema vibaya kila siku; ‘huyu Yusuf huyu, iko siku.’

Kwa tabia hiyo tu, msichana mmoja aliondokea kumpenda sana Yusuf. Nilibaini hilo kwani Yusuf alipokuja kunyang’anywa pikipiki na bosi wake akawa hana mbwembwe tena na uhusiano wake na yule msichana ukafa.

Yusuf hakuwa na pesa za kumhonga huyo msichana, kwani yeye alikuwa akifanya biashara zake, sanasana yeye Yusuf ndiye aliyekuwa akipigwa tafu ya vijisenti.

LAKINI KUNA KUNDI HILI

Kundi ninalopenda kulizungumzia kwa leo ni lile la wanawake hasa, ambao wanaingia kwenye uhusiano wa kimapenzi na wanaume kwa dira zao.

Utakuta mwanamke anamkubali mwanaume kwa sababu tu amehisi atakuwa akipewa pesa nyingi. Au kama mwanaume ana duka, anategemea akimkubali atakuwa akipewa bidhaa za dukani bure.

Wengine ni wale wanaoingia kwenye uhusiano kwa sababu wanaume hao wana vyeo vikubwa au ni mastaa, hawa ndiyo ninaosema mimi kwamba, inapotokea pesa zimekata, hapewi kama zamani, inapotokea cheo kimeisha, inapotokea hali ya biashara inayumba hivyo hapewi mchele kama zamani ndiyo hujuta na kuliona penzi ni chungu.

KUWA KATIKA KUNDI HILI

Siku zote unapotaka kuingia kwenye uhusiano kubali kwa mwanaume ambaye kila ukipima upendo wako kwake unauona hauna sababu yoyote. Yaani humpendei pesa, humpendei cheo wala ustaa, bali unampenda tu! Ndiyo maana wahenga walisema penye penzi la kweli, mwenye chongo huonekana ana makengeza!

Ukipenda kwa mtindo huu, huwezi kuteseka kwani hali yoyote utakubaliana nayo.

Video: Ugomvi wa kimapenzi wamalizikia kwenye gari

Picha za gari lililokuwa na ujumbe wa kukasirisha uliochorowa katika gari hilo zimesambazwa mara elfu katika mtandao wa Twitter. Gari hilo jeupe aina ya Range Rover Revere lenye bei ya pauni 75,000 lilionekana limeegeshwa karibu na Harrods magharibi mwa London na kuchorwa ujumbe wa kukasirisha kwa kile kilichoonekana kuwa mpenzi aliyedanganywa.

Gari hilo liliandikwa ‘cheater’ (mwongo) katika pande zote mbili za gari huku maneno ”Natamani angekuwa na thamani” yakiandikwa katika madirisha ya gari hilo. Kila ambaye alipiga picha za gari hilo alisema kuwa alimuona mwanamke mmoja akilichora gari hilo, alikuwa kama aliye na wazimu.
‘Hakuna mtu aliyejaribu kumzuia. Baadaye aliondoka.Maneno ”Its Over” pia yaliandikwa kwenye gari hilo ikielezea kuisha kwa uhusiano wowote”.

Madhara matatu ya mwanamke kushobokea penzi la pesa!

Mapenzi ni nguzo ya maisha yetu, kama ukifanikiwa kumpata mpenzi ambaye atakupenda na wewe ukampenda ni wazi kuwa maisha yako yatakuwa yenye furaha!

Wakati mwingine unaweza ukapendwa na mpenzi ambaye hujampenda, unadhani kuna ulazima wa wewe kulazimisha kumpenda?

Moyo wako umeshazungumza na wewe, umekuweka wazi kuwa hauna mapenzi ya dhati kwa mtu huyo, kwa nini ujilazimishe eti kwa sababu umeona mtu huyo ana uwezo kifedha?

Kama ulikuwa hujui, ukilazimisha kumpenda mtu kwa kuwa ana mali nyingi, pesa kwake siyo tatizo, ipo siku utajuta hasa pale ambapo utabaini kuwa, huna mapenzi ya dhati na mtu huyo bali tamaa yako ya pesa ndiyo iliyokuingiza huko.

Tatizo hili mara nyingi huwa kwa wanawake! Anatongozwa na mwanaume, mwanaume huyo anajinasibu kwa uwezo wake na jinsi alivyompenda kwa dhati. LaKini kwa bahati mbaya unaweza kukuta msichana huyo wala hana hata chembe ya penzi kwa mwanaume husika.

Lakini kwa tamaa yake, anakubali akijipa matumaini kuwa, atajifunza kupenda akiwa ndani ya penzi. Nani kakudanganya kuwa unaweza kuingia kwenye uhusiano na mtu usiyempenda kisha ukajifunza kumpenda mkiwa ni wapenzi?

Hili ni jambo ambalo haliwezekani na wengi ambao waliingia kwenye uhusiano kwa sababu ya pesa au mali, leo hii ndiyo wanaoongoza kwa kuachika na kusaliti.

Ndiyo! Ni lazima hayo yatokee kwa sababu, kama humpendi bali umependa pesa zake, ukiwa naye ndani ya ndoa lazima utatafuta yule unayempenda kwa dhati na matokeo yake utaanza kuchepuka.
Ukishaanza katabia hako, kwanza utaleta magonjwa ndani ya ndoa, pili kuna siku utabainika na kuambulia talaka kama siyo kipigo lakini tatu utaonekana ni mwanamke ambaye hujatulia.

Sasa kwa nini hayo yakukute? Kwa mwanamke anayejitambua hawezi kuingia kwenye uhusiano na mtu ambaye hampendi. Atafanya mawasiliano na moyo wake kwanza, ukikubali kuwa na mtu huyo ndiyo ataingia lakini moyo ukisita hata kama ameona mwanaume aliyemtokea ana fedha na mali nyingi, atamuacha apite.

Hii yote ni kwa sababu, penzi la dhati ndilo linaloweza kukupa furaha maishani mwako. Ukimpenda mtu eti kisa mali zake, huwezi kuipata ile furaha uliyoitarajia hivyo ni vizuri ukawa makini katika hilo.