Mama Maria Nyerere ataka wabunge waijadili escrow

Mama Maria Nyerere

Mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere amesema wabunge wanatakiwa kuijadili kwa kina ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuhusu Akaunti ya escrow kwa kuwa kuficha mambo kutaendelea kuzidisha matatizo nchini.

Alisema njia pekee ya kulimaliza suala hilo linalotarajiwa kuwasilishwa bungeni leo, ni kwa wabunge kuijadili taarifa hiyo na kuchukua hatua zinazostahili.

Mama Nyerere alisema hayo jana nyumbani kwake Msasani Dar es Salaam, alipojibu maswali ya waandishi wa habari waliotaka kujua maoni yake kuhusu escrow kama suala hilo linatakiwa kujadiliwa au kutojadiliwa bungeni. “Jambo hili sasa liko kwenye magazeti kwa muda mrefu, ningependa lijadiliwe na wabunge limalizike kabisa, lisipojadiliwa tutatafuta matatizo makubwa baadaye,” alisema.

Mama Nyerere alisema suala hilo linagusa masilahi ya umma, hasa katika kipindi hiki ambacho wengi wanakosa huduma muhimu kutokana na uhaba wa fedha unaoikabili Serikali.

“Wanaposikia ripoti za ukaguzi zinafichwafichwa wakati ndugu zao wanakufa kwa kukosa dawa ni lazima watakuwa na hasira na baadaye kusababisha machafuko,” alisema.

Hata hivyo, alisema katika Serikali ya Awamu ya Kwanza kulikuwa na wizi wa mali ya umma lakini hali iliyopo sasa ni ya kutisha.

“Wizi haujaanza leo, hata zamani watu walikuwa wanasogeza fedha za umma, lakini sasa hivi hali imezidi kwenye vyombo vya habari kila siku ni ufisadi, jambo muhimu ni kuchukua hatua haraka,” alisema.

Leave a comment